BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!
Mpendwa rafiki yake Mwenyezi Mungu! Nakuomba upate kulichunguza somo hili ambalo kwa shida sana linaongelewa habari zake. Amani tamu ya Mwenyezi Mungu na Neema yake na iwe pamoja nawe. Kuna ahadi moja katika Kurani Tukufu, inayokuja kwa wale watubuo (Sauti itasema:) “Haya ndiyo mnayoahidiwa, kwa kila aelekeaye (kwa Mwenyezi Mungu), ajilindaye (na maasia). Sura 50:32 QafToba ya kweli ni nini? Nani alazimikaye kutubu? Haya ni baadhi tu ya maswali tunayotaka kuyajibu katika somo hili fupi.
Aina moja ya toba inayo huzuni ndani yake kwa jambo fulani lililotendwa au kusemwa ambalo limeleta huzuni au maumivu kwa mtu mwingine. Inajumuisha sikitiko au maumivu anayojisikia mtu kuhusiana na mwenendo wake uliopita. Mara nyingi toba hii ni matokeo ya hofu ya kuadhibiwa kunakoweza kuja kama matokeo ya matendo ya mtu huyo. Lakini hiyo si toba ya kweli…
Toba ya Kweli
Toba ya kweli ni huzuni inayoingia mpaka ndani au ni kujuta kwa ajili ya dhambi kama chukizo na fedheha kwa Mwenyezi Mungu na huonekana kama ni uvunjaji wa Sheria yake Takatifu ya Amri Kumi. Kwa uweza wake Mwenyezi Mungu, kwa njia ya Roho Mtakatifu, toba hiyo yaweza kuleta badiliko katika maisha. Toba ya kweli ni badiliko la moyo au kuongoka kutoka dhambini na kwenda kwa Mwenyezi Mungu.
Toba ni kuachana kabisa na mazoea yo yote, ukiguswa moyoni kuwa yamemchukiza Mwenyezi Mungu, hata kama tendo hilo limetendwa kwa mtu fulani, lakini bado linaangaliwa kuwa ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu. Toba ya kweli sikuzote ndani yake inatamani kuzitii Sheria Takatifu za Mwenyezi Mungu, yaani, zile Amri Kumi.
Injili yatuambia sisi kuwa “Huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; lakini huzuni ya dunia hufanya mauti.” 2 Wakorintho 7:10
Toba ya kweli ni wakati ule mtu, kwa njia ya Roho Mtakatifu au Ruh wa Mwenyezi Mungu, anasadikishwa ya kwamba anawaza au anatenda lile ambalo limesababisha kuzivunja amri zake Mwenyezi Mungu. Aguswapo sana moyoni, ndipo anafanya maamuzi kumfuata Mwenyezi Mungu kikamilifu na tena anaamua kuishi maisha yake yote kwa ajili ya Mungu. Mwenye dhambi anageuka na kuacha maovu yote ayajuayo moyoni mwake na katika maisha yake kwa nguvu anazopewa na Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo toba ya kweli.
Nabii Masihi Isa alikuwa na mengi ya kusema juu ya toba. Humu katika Injili imeandikwa: “Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.” Injili Marko 2:17. Inasema wazi sana kwamba Masihi Isa aliwaita wenye dhambi ili watubu. Hii inatuhusu sisi sote, kwa maana wanaume na wanawake wote wanahitaji toba.
Toba ya kweli huleta matengenezo!
Toba ya kweli iliyonenwa katika Kurani Tukufu yahusu kuachana kabisa na maisha ya dhambi na kuishi maisha ya kumcha Mungu. Yohana au Yahaya aliyemtangulia Masihi Isa alihubiri toba inayowatoa watu dhambini. “Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.” Injili Luka 3:3.
Ulikuwa na nguvu kweli ujumbe ule wa Yohana… “Basi, toeni matunda yapatanayo na toba; wala msianze kusema mioyoni mwenu, Tunaye baba, ndiye ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba katika mawe haya Mungu aweza kumwinulia ibrahimu watoto.” Injili Luka 3:8. Masihi Isa alithibitisha tena kuwa alikuja kuwaita wenye dhambi ili watubu. “Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu.” Luka 5:32.
“Na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanzia tangu Yerusalemu.” Luka 24:47
Ujumbe huo uliwajia Israeli ya Kale: “Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini [tubuni], mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu.” Taurati Ezekieli 18:30
Ishara za Toba ya Kweli!
Katika nyakati zile za zamani Taurati inasema juu ya watu wa Ninawi waliogeuka na kuwa waovu kupindukia. Mpaka hapo walikuwa wameziacha njia zake Mwenyezi Mungu hata akawatumia ujumbe kupitia Nabii Yona (Yunus). Njia za uovu wao zilikuwa zimezama chini sana hata Mwenyezi Mungu akafanya ujumbe upelekwe kwao uliowatikisa sana. “Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.” Yona 1:1-2.
Katika kisa kifuatacho angalia ishara maalumu walizofanya watu wale wa Ninawi kuonesha toba yao ya kweli.
“Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, ‘Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.’ Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga; wakijivika nguo za magunia [maturubai], tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, ‘Kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilia Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mkononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili tusiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.” Yona 3:4-10.
Watu wale wa Ninawi walionesha ishara za kweli za toba kwa kubadilisha maisha yao kwa dhati. Ujumbe wa Yona uliwafanya wamtafute Mungu kwa moyo mnyofu. Kuanzia mtawala mwenye nguvu sana kwenda chini mpaka kwa wanyama wanyonge walikuwa wamevaa maturubai, wakatangaza saumu, na kuketi katika majivu kama ishara ya unyenyekevu wao kwa Mungu.
Wakasisitiziwa kuacha njia zao mbaya na za uovu na kumwomba Mwenyezi Mungu ili awahurumie. Mwenyezi Mungu akazisikia dua zao na kuona toba yao ya kweli na historia yatufunulia kwamba Ninawi, mji ule wa kale, uliepushwa wasiangamizwe kwa miaka mingine 140. Mungu kwa rehema zake atazisikia dua zetu na kuiona toba yetu.
Mwenyezi Mungu Aahidi kutupa Moyo Mpya
“Basi, nitawahukumu ninyi, nyumba ya Israeli, kila mmoja kwa kadiri ya njia zake, asema Bwana MUNGU. Rudini, mkaghairi, na kuyaacha makosa yenu yote; basi hivyo uovu wenu hautakuwa uharibifu wenu. Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mliyoyakosa; jifanyieni moyo mpya na roho mpya; mbona mnataka kufa, asema Bwana MUNGU; basi ghairini, mkaishi.” Taurati Ezekieli 18:30-32. Wito wa Mwenyezi Mungu wa kutubu ni kwa watu wote wa kila taifa.
“‘Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia Roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda.”
Taurati Ezekieli 36:24-27
Basi wengine waweza kuuliza hivi, inakuwaje hata mtu aweze kutubu? Je, jambo hilo latokana na yeye mwenyewe? Hapana, kwa kuwa ile nia ya mwili ni uadui juu ya Mungu. Basi, moyo wa asili wawezaje kujichochea wenyewe hata upate kutubu wakati hauna uwezo wa kufanya hivyo? Ni kitu gani kinachomfikisha mtu kwenye toba? Ni Masihi Isa. Je, anamfikishaje mtu kwenye toba? Kuna njia elfu moja awezazo kuzitumia kufanya hivyo, sisi twahitaji tu kuomba.
Karama ya Mwenyezi Mungu ya Toba!
“Akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana Mungu awape kutubu na kuijua kweli.” 2 Timotheo 2:25
“Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.” 2 Petro 3:9
“…Wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu…” Warumi 2:4
Ni kweli iliyoje, basi, kwamba ni Neema nyingi ya Mwenyezi Mungu inayotuvuta tupate kutubu. Sisi wenyewe kama binadamu hatujui hata jinsi ya kutubu. Ni dhahiri tunasikia huzuni au hatia ya dhambi, lakini jinsi ya kugeuka, yaani, jinsi ya kugeuka kabisa katika maisha yetu na kwenda mbali na dhambi mioyoni mwetu, hiyo ni kazi ya Mwenyezi Mungu tu. Wengi kwa mwenendo wao wa nje wataepuka maovu na dhambi nyingi, lakini kama moyo ungechunguzwa ingegunduliwa ya kuwa ndani ya mioyo yao bado wanatamani tendo lile ovu. Ndani ya moyo dhambi ile haijaondolewa, bado imo mle, tena inapendwa sana. Kadiri dhambi inavyozidi kupendwa bado inatushikilia sisi mateka. Ni lazima dhambi iondolewe moyoni kabla mtu hajawa huru.
Yatupasa kuomba tupewe karama ya toba ya kweli, naye Mwenyezi Mungu atatupa. Kumbukeni Isa alipokuja duniani, hakuna mtu hata mmoja aliyekwenda zake bila kutimiziwa ombi lake, lakini wote waliponywa, itakuwa hivyo kwetu pia, ombi letu liwalo lote kuhusu kuiponya mioyo yetu yenye dhambi litajibiwa. Laiti kama tungemwomba tu Mwenyezi Mungu katika maisha yetu ya faragha, yeye ayatunzaye malimwengu pamoja na kuliongoza kundi kubwa la nyota ikiwamo na dunia yetu katika mzunguko wake, anao pia muda na shauku kwa kila mmoja wetu leo hii. Hakuna mtu hata mmoja asiyeonwa naye, hakuna aliye mdogo mno hata asiweze kumwona, naye anangoja kutoa Neema yake hata kwa yule aliye mdogo kabisa. Mpendwa rafiki yake Mwenyezi Mungu, tumwombe leo hii atupe karama ya toba, ili maisha yetu yaweze kuoshwa uchafu wa dhambi kwa njia ya Isa. www.salahallah.com
“Kumgeukia Mwenyezi Mungu kwa Toba ya Kweli”
Sura 50:32 Qaf
Mfululizo na.38