Kiswahili 32. “Nguo za utawa [zifunikazo]” sehemu ya kwanza

BISMILA-HIR RAHMA-NIR RAHIM

Asalamu Aleikum!
Salamu katika jina lake Mwenyezi Mungu, mwenye rehema nyingi sana na mwenye haki, anayesamehe mara nyingi na mwenye huruma. Roho (Ruh) wa Mwenyezi Mungu awe nanyi mnapolitafakari somo hili ambalo ni la muhimu mno kwetu kulijua!

 

“Enyi wanadamu! Hakika tumekuteremshieni nguo zifichazo tupu zenu na nguo za pambo, na nguo za utawa (yaani kucha Mungu) ndizo bora.” Hayo ni katika ishara zake (neema za) Mwenyezi Mungu ili wapate kukumbuka.”
Sura 7:026 Al Aaraf

Haki (utawa) bila shaka ni somo la maana, kwa kuwa limetajwa zaidi ya mara 70 katika Kurani Tukufu na zaidi ya mara 200 katika Biblia. Hivi “haki” maana yake nini? Maana iliyo dhahiri ya neno hili ni:
“Usafi wa moyo na uadilifu wa maisha, moyo na maisha yale yanayotii sheria ya Mungu. Haki, kama neno hilo litumikavyo katika Maandiko/Kurani na theolojia, ambamo linatumika sana, linakaribia sana kuwa sawa na utakatifu, yaani, kuzijua kanuni takatifu na mapenzi ya moyo, na maisha yafuatayo sheria ya Mungu. Inajumuisha yote tuyaitayo haki mbele ya sheria, yaani, unyofu wa moyo na wema, kuwa na mapenzi matakatifu, kwa kifupi, hii ndiyo dini ya kweli.”

Basi, twaipataje hiyo “haki”? Je, hivi sisi kwa asili yetu tunayo tabia kama hiyo maishani mwetu?

Adamu na Hawa
Wazazi wetu wale wa kwanza walibarikiwa kwa kuwa na haki katika ile Bustani. Walifanywa kuwa wenye haki, tangu walipoumbwa.…Ilikuwa ni zawadi iliyotoka mbinguni, lakini mara tu walipotenda dhambi waliipoteza zawadi hiyo ya haki. Kwa maneno mengine, walipoyasikiliza madanganyo yake Ibilisi badala ya kulisikiliza Neno la Mwenyezi Mungu wakaanguka kutoka katika haki. Basi, wazao wote wa Adamu hawana njia yo yote ya kuipata tena, isipokuwa kama wakipewa na Mungu. Hatuna wema wo wote katika maisha yetu haya…Wema wetu wote/haki yetu yote ilipotea mwanadamu alipotenda dhambi katika ile bustani. Sisi hatuna haki hiyo kabisa. Wala hatuna wema wo wote ndani ya mioyo yetu, wala hatuwezi kustahili kupata hiyo haki kwa matendo yetu mema.

“Kama ilivyoandikwa, Hakuna mwenye haki hata mmoja.” Injili Warumi 3:10

Kama ilivyoelezwa nyuma katika ile bustani ya Edeni, Adamu na mkewe, wote wawili walikuwa wenye haki. Hawakuwa na haja ya kuwa na nguo zo zote za kujifunika wenyewe, kama ishara ya haki yao walifunikwa na vazi la nuru. Nabii Daudi aliandika hivi:
“Ataitokeza haki yako kama nuru, na hukumu yako kama adhuhuri.”
Zaburi 37:6
Hapo haki ni sawa na Nuru. Hivyo wazazi wetu wale wa kwanza hawakuvaa nguo zo zote zilizotengenezwa na wanadamu, walivikwa nuru. Adamu na Hawa walipoanguka kutoka katika haki, walilipoteza vazi lao lile la mbinguni lililowafunika na, sasa, wakajiona wenyewe kuwa wako uchi na ile nuru hawakuwa nayo kabisa. Walikuwa wameusikiliza uongo wa Ibilisi, na lile vazi la nuru lililowafunika likatoweka. Katika Kurani
Tukufu inaeleza hivi…
“Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Peponi (humo). Na Adamu akamkosa Mola wake, na akapotea kidogo njia.” Sura 20:121 Ta Ha

Mungu alipokuja akiwatafuta wakajificha… nao wakajaribu kujifunika wenyewe kwa majani, kuficha uchi wao.
“Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo. Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini nikaogopa wa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.”
Taurati Mwanzo 3:7-10

Vazi Lifunikalo la Mungu
Katika kuchanganyikiwa kwake Adamu kwa kujikuta yu uchi, ilibidi Mungu amfunike kwa ngozi za wanyama. Ilikuwa lazima achinjwe mwana-kondoo ili kutengeneza mavazi ya mwanamume yule na mkewe ambao walikuwa uchi. Ilikuwa ni lazima damu imwagwe ili mwanadamu yule apate tena vazi lile lifunikalo. Hayo yote yalielekeza mbele kwa yule Mwana-Kondoo wa Mungu ambaye siku moja angekuja kuzichukua dhambi za ulimwengu. “…Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu.” Injili Yohana 1:29

Hivyo [Isa] Kristo alikuwa Kondoo wa Mungu, na ilikuwa damu yake iliyomwagika ili mwanadamu mwenye hatia aweze kusamehewa dhambi zake, na mara moja tena aipate ile haki. Mwanadamu angeweza tu kwa njia ya Yesu kuufunika tena uchi wake kwa Haki ya Masihi Isa, yaani, Yesu.
Vazi la ngozi lililowafunika lilikuwa ni la muda mfupi tu. Mwanadamu alipewa nafasi ya pili ili kuipata ile haki iliyopotea.
Lakini, basi, ni kwa jinsi gain mwanadamu angeweza tena kuipata tabia ya utakatifu iliyopotea? Mwanadamu alikuwa ameupoteza uwezo wake wa kufanya mema. Asingeweza kabisa kwa uwezo wake mwenyewe kufanya mema au kuwa mtakatifu moyoni mwake. Ni utata ulioje huo mwanadamu aliojiingiza ndani yake! Msaada ungetoka wapi?

Mungu alikuwa na mpango… katika mpango wake, angempa tena lile vazi takatifu lifunikalo. Vazi lile lingetoka kwa mwanadamu mwingine… Adamu wa pili… yaani, Kristo.

“…Nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki…” Isaya 61:10.
“Haki yako ni haki ya milele, na sheria yako ni kweli.”
Zaburi 119:142

Haki ni kitu fulani tulichokipoteza, lakini tunapomtii Mungu, na kumwamini Kristo, anatuvika tena hilo vazi. Hilo hufanyika kupitia Isa aliyeteremshwa… zingatia ya kwamba haki ni kama vazi tulilovikwa…
Ayubu, mtu mmoja kutoka miongoni mwa watu wale wa Mashariki wenye hekima kweli kweli, alisema… “Nalijivika haki, ikanifunika, adili yangu ilikuwa kama joho na kilemba.” Taurati Ayubu 29:14.”
“Kwa maana ikiwa kwa kukosa mtu mmoja [Adamu] mauti ilitawala kwa sababu ya yule mmoja, zaidi sana, wao wapokeao wingi wa neema, na kile kipawa cha haki, watatawala katika uzima kwa yule mmoja, Yesu Kristo.” Injili Warumi 5:17.”

“Ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti.” Injili 3:22

Ee mpendwa msomaji, je, utakiamini na kukipokea kipawa (zawadi) hiki cha haki kutoka kwa Mungu? Hicho ni zawadi, wala hakiwezi kupatikana kwa kufanya kazi. Vinginevyo kinakoma kuwa zawadi.

“Sio wema (tu huo peke yake) kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa Mashariki na Magharibi (katika kusali. Yako na mema mengine). Bali wema (hasa) (ni wa wale) wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu [Biblia] na Manabii…”
Sura 2.177 Al Baqarah

Tunaagizwa kuitafuta Haki. Ni dhahiri kwamba inaweza kupatikana, vinginevyo tusingeagizwa kuitafuta.

“Mtafuteni BWANA, enyi nyote mlio wanyenyekevu wa dunia, ninyi, mliozitenda hukumu zake, itafuteni haki, utafuteni unyenyekevu; huenda mtafichwa katika siku ya hasira ya BWANA.” Sefania 2:3.”
“Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Injili Mathayo 6:33
“Heri wenye njaa na kiu ya haki; maana hao watashibishwa.”
Injili Mathayo 5:6

Hiyo ni kwa ajili ya wote, kwa kila taifa… kwa kila mtu duniani. Ahadi zake ni za hakika.
“Haki huinua taifa; Bali dhambi ni aibu ya watu wote.” Mithali 14:34

Twaambiwa katika Kurani Tukufu ya kwamba Isa alikuwa kipawa cha mwana mwenye haki. [Sura 19:19]. “Kurani Tukufu” Alidumisha uadilifu wake mbele za Mungu na sasa akapata haki ya kutupa sisi tunaomwamini zawadi hiyo ya thamani.
Kwa hiyo ni kweli kwamba matendo mema ni matokeo ya kipawa hicho cha Haki tulichopewa. Kwa hiyo, matendo mema yanayotoka moyoni ni tunda la haki. Mara tu sisi tunapokuwa na kipawa hiki tunayo haki kamili ya kuingia Mbinguni. Hivyo yote hutegemea juu ya kukipata kipawa hiki cha Haki, kwa kweli kinafanana na vazi… nasi yatupasa kuvikwa vazi hili la mbinguni. Limefumwa katika kiwanda cha mbinguni bila kutumia ubunifu wa kidunia. Vazi hili litakupa wewe nafasi kubwa ya kuingia katika ufalme wenye Nderemoi nyingi.
“Mmoja ataniambia, kwa BWANA, peke yake, iko haki na nguvu… Isaya 45:24

Haki na sheria sikuzote huenda pamoja. Haviwezi kutenganishwa.
“Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari.” Taurati Isaya 48:18
“Ulimi wangu na uiimbe ahadi yako, maana maagizo yako yote ni ya haki.”
Zaburi 119:172
“Bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.” Injili Matendo 10:35
“…na jina lake atakaloitwa ni hili, BWANA NI HAKI YETU.”
Yeremia 23:6
Katika siku za mwisho, Wakristo wa kweli na Waislamu wa kweli wataungana na kwa pamoja watatangaza sifa za Mwenyezi Mungu na kupokea Haki yake.
“Maana kama nchi itoavyo machipuko yake kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.” Taurati Isaya 61:11
“Na walio na hekima watang’aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang’aa kama nyota milele na milele.” Danieli 12:3
Leo hii mwombe Mwenyezi Mungu ili uweze kuwa na vazi lifunikalo la Haki ambalo linatoka kwa Isa.
Kwa maelezo zaidi, tafadhali wasiliana nasi:
www.salahallah.com

“Nguo za Haki”
Sehemu ya Kwanza

Sura 7:26
Al Aaraf

Mfululizo na.32